Chimbuko
Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika ilibuniwa na Tanzania mwaka 2003 kwa tathmini iliyofanywa na wadau wa urithi wa ukombozi wa Afrika. Pamoja na Tanzania kuongoza harakati za ukombozi wa Afrika hapakuwa na vielelezo na ushahidi uliothibitisha bayana kuhusu historia ya ukombozi huo. Kutokana na tathmini hiyo, Chama cha Mapinduzi na wadau wa urithi (UNESCO) waliona kuna umuhimu wa kuanzisha Programu ili kuhifadhi Urithi wa Ukombozi wa Afrika. Wazo hili lilikubaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2004, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNESCO ilituma ujumbe wa Tanzania kwenda Angola, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. Katika ziara hiyo, ilikubalika kwamba utekelezaji wa Programu hiyo ujumuishe nchi zote za Kusini mwa Afrika na kusimamiwa na Tanzania.
Kufuatia hatua hiyo, Mkutano wa wadau uliofanyika Dar es Salaam ambao uliamua Programu hii iwasilishwe UNESCO, Shirika ambalo linahusika na Utamaduni na uhifadhi wa urithi wa Dunia. Mwaka 2005, Tanzania iliwasilisha pendekezo hilo kwenye Mkutano Mkuu wa 33 wa UNESCO na kuungwa mkono na nchi 11 za Afrika ambazo ni: Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. Mkutano huo uliridhia pendekezo hilo na kujumuisha Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika katika mpango mkakati wake wa miaka minne kuanzia 2008-2012
Halikadhalika, mikutano mingine ya mashauriano ya Kimataifa ilifanyika kuunga mkono wazo la uanzishwaji wa Programu ikiwemo: Mkutano wa Kimataifa wa Mashauriano uliofanyika Windhoek, Namibia (2008), Mkutano wa Mawaziri wa Utamaduni wa nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika Algiers, Algeria (2008) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali na Wenyeviti wa vyama vilivyoongoza harakati za ukombozi uliofanyika, Dar es Salaam 2010
Mikutano hiyo ilisisitiza umuhimu wa kujumuisha nchi zote za Afrika kwenye Programu hiyo. Mwaka 2011, pendekezo hilo liliwasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya ridhaa na maelekezo yao. Mkutano huo uliridhia utekelezaji wa Programu na kukubaliana Makao Makuu yake yawe Dar es Salaam, Tanzania.
Hivyo, chimbuko la Programu linatokana kuwepo kwa urithi wa ukombozi unaohitaji kutambuliwa, kuhifadhiwa na kutangazwa ambao ni pamoja na: (picha, filamu, simulizi, barua, hotuba za Viongozi, machapisho, nyaraka, maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru, nyimbo, sare, michoro, ramani za maeneo ya ukombozi, mahandaki, zana) ambao ulitokana na harakati za Ukombozi wa Afrika.