ASA KUSHIRIKIANA NA TFC ILI KUONGEZA UZALISHAJI NA USAMBAZAJI WA MBEGU BORA ZA KILIMO NCHINI
26 Mar, 2025
ASA KUSHIRIKIANA NA TFC ILI KUONGEZA UZALISHAJI NA USAMBAZAJI WA MBEGU BORA ZA KILIMO NCHINI

Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) wamefanya kikao cha pamoja kujadili namna ya upatikanaji wa mbolea na usambazaji wa mbegu bora za kilimo nchini. 

Akiongoza kikao hicho Mkurugenzi wa Uzalishaji wa ASA Dkt. Justin Ringo, Makao Makuu ya ASA mjini Morogoro, amesema wanafanyia kazi maagizo ya Wizara ya kuhakikisha ASA na TFC zinafanya kazi kwa karibu na kwa tija zaidi. Aidha, amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujadili kwa pamoja namna ya kushirikiana katika upatikanaji wa uhakika wa mbolea kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na usambazaji mbegu kwa wakulima kupitia vituo vya usambazaji wa mbolea vya TFC nchini. 

“Tuna mashamba 13 ambayo yanayozalisha mbegu bora za kilimo mikoa mbalimbali na kufanya mahitaji ya mbolea kuwa makubwa, hivyo kila mwaka malengo ya uzalishaji yanaongezeka na kufanya mahitaji ya mbolea kuongezeka pia” amesema Dkt Ringo.

Aliongeza kuwa, "majadiliano kati ya taasisi hizi mbili yatawezesha upatikanaji wa uhakika zaidi wa mbolea na pia kurahisisha mbegu kuwafikia wakulima wengi nchini kwa wakati". 

Aidha, Mkurugenzi wa Maendeleo wa TFC Bw. Lameck Bonega amesema kikao hiki ni matokeo ya maelekezo ya Mhe. Hussein Bashe Waziri wa kilimo juu ya ushirikiano wetu TFC na ASA, kutumia vituo vya usambazaji wa mbolea vilivyopo nchini ili kuwezesha upatikanaji wa mbolea kwenye mashamba ya ASA na kuwezesha usambazaji wa mbegu bora za kilimo kuwafikia wakulima kwa wakati.

Pia, kikao hiki kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka ASA wakiwemo Mameneja Sehemu ya Mashamba, Sehemu ya Masoko, Kitengo cha Sheria, Mhakiki wa Ubora wa Mbegu na wajumbe wengine kutoka TFC akiwemo  Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Biashara wa TFC pamoja na Mwanasheria.