Tanzania emblem

Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika

Urithi wa Ukombozi, Fahari ya Afrika

Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika

Habari

Mitaala ya Elimu inayoandaliwa kuzingatia Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika


Kituo Cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, kilichopo Chini ya Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wametekeleza agizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo kupitia vikao vyake ilielekeza Wizara ya Utamaduni kuhakikisha mitaala inayoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania kuzingatia na kuingiza maudhui ya Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika hususani Mchango wa Tanzania katika kusaidia Uhuru wa Nchi za Afrika.

Kikao hicho, pamoja na masuala mengine kimepitia mitaala hiyo na kujiridhisha kuwa maudhui ya Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika hususani Mchango wa Tanzania katika kusaidia Uhuru wa Nchi za Afrika yamezingatiwa katika Rasimu ya mitaala ya ngazi mbalimbali za Elimu.

Hata hivyo, Kikao hicho kimejadili kuboresha zaidi maeneo hayo ya mitaala kwa kuongezea kilichopungua ili Kuenzi Historia hiyo ambayo ni Tunu kwa Tanzania na Afrika.

Sambamba na Hilo Kikao kimeazimia kuandaa MOU baina ya Taasisi ya Elimu na Kituo Cha Urithi wa Ukombozi ili kutekeleza maelekezo hayo na kuwa na Ushirikiano wa Kudumu.

Kikao hicho kimeratibiwa na Wizara ya Utamaduni na Mwakilishi wa Katibu Mkuu alikuwa,

Mratibu wa Kituo Cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Bw. Boniface Kadili huku Wizara ya Elimu ikiwakilishwa na Menenjimenti ya Taasisi ya Elimu Tanzania ikiongozwa na

Mkurugenzi wa Taasii hiyo, Dkt. Aneth Komba.