Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan afanya ziara ASA katika shamba la Mbegu la Msimba.
05 Aug, 2024
Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan afanya ziara ASA katika shamba la Mbegu la Msimba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Kilimo kuanza mchakato wa kutunza Mbegu za Asili.

Rais Samia amesema hayo katika ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro wilaya ya Kilosa katika Shamba la Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Msimba. Amesisitiza kuwa wizara ya Kilimo kupitia Taasisi zake ianze mchakato wa kutunza Mbegu za Asili ili kulinda Mbegu hizo zisipotee maana ni hazina kubwa kwa jamii.

Mhe.Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan amekagua Kiwanda Cha kisasa cha kuchakata Mbegu Cha ASA chenye uwezo wa kuchakata Tani 4 kwa saa. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata Mbegu mbalimbali kama vile Mahindi, Alizeti,Mtama,Ngano pamoja na Mazao jamii ya Mikunde.

Dkt.Samia ameipongeza Taasisi ya Wakala wa Mbegu za kilimo ASA kwa kuendelea kuzalisha Mbegu bora za kilimo na kuuza kwa wakulima kwa bei nafuu.

Awali ya hapo Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe alimweleza Mhe. Rais kuwa, ASA imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya Umwagiliaji ambapo kwa sasa zaidi ya hekta 3,000 zimetangazwa kwenye mfumo wa serikali 
kwa ajili ya kuwekewa mindombinu ya umwagiliaji mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Waziri Bashe amesema Wakala wa Mbegu bado unahitaji Mashamba yenye miundombinu muhimu ili kuweza kufikia Malengo ya Uzalishaji wa Mbegu bora na kupunguza uagizaji wa mbegu kutoka nje ya nchi.

Bashe amemwambia Mhe.Rais Uzalishaji wa Mbegu umeongezeka kutoka Tani 3000 hadi kufikia Tani 49,000 huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya Tani 127,000.

Aidha kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Bwn.Leo Mavika akitoa maelezo kwa Mhe. Rais dhidi ya matumizi ya Kiwanda hicho amesema Kiwanda kina uwezo wa kuchakata Mbegu Tani 4 kwa saa.

Amesema Kiwanda hicho kitawezesha Mbegu zinazozalishwa kuwa na ubora zaidi. Vile vile amesema kiwanda hicho ni moja ya mikakati yake ya kuongeza tija na kupunguza gharama zilizokuwa zinatumika kusafirisha mbegu kwenda Makao makuu Morogoro kwa ajili ya kuchakatwa.

Mavika amesema Wakala utaendelea kutekeleza maagizo yote ya serikali ili kufikia Malengo yanayotarajiwa.