KAMATI YA BUNGE YAKOSHWA NA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI ASA

Kamati ya kudumu ya Bunge ya hesabu za serikali imeridhishwa na matumizi ya Bilioni 15.7 kwa ujenzi wa miundombinu ya Umwagiliaji Hekta 800 katika mashamba ya Wakala wa Mbegu za kilimo ASA .
Akizungumza na waandishi wa Habari leo Machi 23, 2025, katika ziara ya ukaguzi wa Miradi ya ASA Jijini Arusha, Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya hesabu za serikali Mhe. Japhet Hasunga amesema Kamati hiyo imeridhishwa na Miradi ya Uwekaji miundombinu wa Umwagiliaji wa hekta 200 unaotekelezwa katika Shamba la Mbegu Arusha lililopo Ngaramtoni. Aidha, hekta 200 pia zinatekelezwa katika shamba la Mbegu Msimba lililoko Kilosa Mkoani Morogoro pamoja na hekta 400 katika Shamba la Mbegu Kilimi Nzega Tabora.
“Tunaipongeza wizara ya kilimo kwa kuwa wabunifu na mipango madhubuti ya kuhakikisha inaongeza Uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwekeza katika sekta ya Umwagiliaji, Wakala inapaswa kujitangaza kwa kutoa elimu kwa wananchi ili kuwa na soko kubwa la mbegu ikiwa ni pamoja na kutafuta soko la Nje ya nchi hatikaye kuongeza kipato cha kujiendesha vizuri Zaidi” amesema Mheshimiwa Mwenyekiti Husanga
Pia, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA Bwn, Leo Mavika ameipongeza Kamati hiyo kwa kukagua Miradi ya Umwagiliaji na kutoa kuridhishwa na ujenzi unaoendelea.
“Wakala wa Mbegu tutaendelea kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali katika Miradi ili lengo la serikali la kuongeza uzalishaji mbegu bora nchini liweze kutimia kwani mahitaji ya Mbegu Nchini ni Tani 127,650 ambapo upatikanaji wake bado hautoshelezi hivyo jitihada za kuhakikisha Uzalishaji wa Mbegu zinaendelea kwa kuimarisha Umwagiliaji” amesema Bw. Mavika
Aidha ameiambia kamati hiyo kuwa katika Shamba la Mbegu Arusha eneo lililowekewa miundombinu ya Umwagiliaji ni Hekta 160 kati ya 200 sawa na asilimia 82 ya utekelezaji. Shamba la Mbegu Kilimi eneo lililowekewa miundombinu ya Umwagiliaji ni Hekta 220 kati ya 400 sawa na asilimia 60 huku Shamba la Mbegu Msimba uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la hekta 200numefikia asilimia 70.
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu wizara ya kilimo Dkt.Hussein Mohamed Omary amesema kama wizara wataendelea kusimamia maelekezo yote ya Kamati kwa Taasisi zake ili kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri.
Amesema ukamilishaji wa Miradi hiyo mkubwa ya Umwagiliaji itaongeza tija kubwa ya Uzalishaji wa Mbegu Nchini nakupunguza uagizaji wa Mbegu kutoka nje ya nchi.