KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA (PIC) YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA ASA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) leo tarehe 11 Januari 2025 imetembelea Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu (ASA) ikiwa ni ufuatiliaji kutokana na kikao cha Kamati kilichofanyika tarehe 08 Januari 2025 Bungeni Jijini Dodoma ambapo pamoja na kujionea kazi mbalimbali zinazofanywa na Wakala huo katika kuleta mageuzi ya kilimo nchini, Kamati hiyo imetembelea maghala ya Kiwanda cha Mafuta ambayo kwa muda mrefu yamekuwa hayatumiki.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini amesema Serikali inapaswa kukaa na mwekezaji ili kumaliza mgogoro uliopo dhidi ya mwekezaji na maghala hayo yaanze kutumika kuhifadhia mbegu za Wakala wa Mbegu za kilimo ASA ambayo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maghala ya kuhifadhia mbegu.
"Ni lazima Serikali ihakikishe Wakala wa Mbegu ASA anapata maghala makubwa zaidi kwa ajili ya kuhifadhia mbegu wanazozalisha lakini jambo la pili Serikali ihakikishe ASA anapata mitambo mizuri ya kisasa ili aweze kuzalisha mbegu kwa kasi kubwa zaidi." ameeleza Mhe.Augustine Vuma Holle.
Nae Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Nyasebwa Chimagu ameeleza kuwa Wakala wetu wa Mbegu za Kilimo ASA imeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na Serikali inaichukulia ASA kama kichocheo cha ukuaji wa tasnia ya mbegu hapa nchini kwa kuhakikisha uzalishaji wa mbegu lakini pia tija katika uzalishaji.
"Katika Mkoa wa Morogoro kutokana na fursa zilizopo kuna miundombinu muhimu mojawapo ni viwanda ambavyo vilikuwepo ambavyo vinaweza kutumika katika shughuli za kilimo lakini pia yapo maghala ambayo yanaweza kutumika kutumika kwa ajili ya uhifadhi wa mbegu na mazao ili kufikia lengo la kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani million tatu za mazao ifikapo mwaka 2030." ameongeza Bw. Nyasebwa.
Aidha, Bw. Nyasebwa ameeleza kuwa Wizara imeendelea kujenga maghala katika mashmba mbalimbali ya ASA lakini pia tumeendelea kutumia fursa zilizopo Serikalini ambazo ni miundombinu ambayo imekuwepo huko nyuma imelala ama ilikuwa ndani ya Serikali au imewekwa kwa watu wa Sekta Binafsi Wizara inaendelea kuangalia fursa na rasilimali zilizopo Serikalini ambazo hazitumiki ili kuzitumia.
Akizungumza kwa Niaba ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji amesema.Lighthess Mauki ambaye ni Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina amesema Ofisi ya Hazina itaendelea na mazungumzo hayo kama Kamati ya kudumu ilivyo shauri ili maghala hayo yaweze kuanza kutumika.