Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe atembelea Shamba la Mbegu la Msimba la Wakala wa Mbegu Za Kilimo (ASA) na Kutoa maelekezo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu
BASHE ATOA MAELEKEZO KWA MTENDAJI MKUU WA ASA.
Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Bwn. Leo Mavika kutangaza tenda za kuweka Miundombinu ya Umwagiliaji katika Shamba la Mbegu Msimba hekta zaidi ya 2000.
Amesema hayo wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Shamba la Mbegu Msimba wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kuwa Shamba hilo litangazwe.
Amesema Wizara kupitia Wakala wa Mbegu za kilimo ASA imeweka mpango wa kuhakikisha Mashamba ya Wakala yanakuwa na Umwagiliaji wa uhakika ili kuongeza tija ya Uzalishaji wa Mbegu bora nchini.
Aidha Mhe.Bashe amesema Malengo ya serikali ni kuongeza tija ya Uzalishaji wa mbegu kupitia mifumo ya Umwagiliaji.
Akiendelea kutoa maelekezo Waziri amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu Mavika kuhakikisha anaweka mpango mzuri wa matengenezo ya matrekta matatu yaliyopo shambani hapo ili msimu huu wa Kilimo yaingie shambani tayari kwa kilimo.
Amesema Matrekta hayo hayahitaji fedha nyingi za matengenezo hivyo ni lazima yatengenezwe kwa wakati ili kuepusha kukodi au kuhamisha kutoka mashamba mengine .
Mhe.Bashe alitembelea mtambo wa kisasa wa kuchakata Mbegu za kilimo wa Shamba hilo ambapo ameridhishwa na ufanisi wa mtambo huo.
Kwa upande mwingine Bashe alimwagiza kaimu Mtendaji Mkuu Leo Mavika kumwandikia barua haraka ya kumtaka mkandarasi Pro agro global anayefanya kazi ya kuweka Miundombinu ya Umwagiliaji kufika katika shamba hilo ifikapo Julai 28 Mwaka huu ili kuendelea na majukumu ya uchimbaji wa bwawa.
Amewataka watumishi wa Shamba hilo kutunza miundombinu hiyo ya kisasa ya shamba hilo ambalo ni miongoni mwa Mashamba mkubwa ya serikali ya Uzalishaji wa Mbegu bora .
Aidha kwa upande wake kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Bwn. Leo Mavika amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo kulingana na umuhimu wake.
Amesema hekta 300 katika Shamba la Mbegu Msimba zinawekewa miundombinu ya Umwagiliaji na kazi inaendelea.
Bwn. Leo Mavika amesema maagizo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa haraka iwezekanavyo ili kuleta ufanisi wa Uzalishaji wa Mbegu pamoja na kwenda na Kasi ya Uzalishaji.
Mavika amesema Wakala wa Mbegu za kilimo ASA unaipongeza Wizara ya kilimo kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wakala hasa kutoa maelekezo yenye mlengo wa kuongeza tija.