ASA YAKUTANA NA WAKULIMA WA MKATABA ZAIDI YA 80.
ASA YAKUTANA NA WAKULIMA WA MKATABA ZAIDI YA 80.
Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) imeingia makubaliano na wakulima wa mkataba zaidi ya 80 kwa kuzalisha Mbegu za kilimo zaidi ya Hekta 3,140 sawa na Ekari 7,850 zitakazolimwa na wakulima wa mkataba kwa kuzalisha Mbegu bora za kilimo.
Akifungua Kikao hicho cha makubaliano ya Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Bwn. Leo Mavika amesema moja ya majukumu ya Wakala wa Mbegu za kilimo ni kufanya kazi na Taasisi Binafsi hasa katika Uzalishaji wa Mbegu.
Kikao hicho kimefanyika October 15 mwaka huu Mkoani Morogoro lengo likiwa ni kuhakikisha wakulima hao wanaingia mkataba na Wakala wa kuzalisha Mbegu bora kwa kufuata taratibu na kanuni za Uzalishaji wa Mbegu.
Amesema makubaliano hayo yote yanawekwa kisheria ili kila pande iheshimu makubaliano hayo ambayo yanalenga kuongeza Uzalishaji wa Mbegu.
Amesema Wakala itazingatia na kufuatilia kila kipengele katika mikataba ili kuhakikisha kila upande unawajibika ipasavyo ambapo lengo ni kuongeza tija katika Uzalishaji.
Kaimu Mtendaji Mkuu Bwn. Leo Mavika aliendelea kusema baadhi ya wakulima wa mkataba wamekuwa na kasumba ya kuchukua maeneo makubwa na kushindwa kulima hali inayopelekea Taasisi kutofikia malengo kama ilivyotarajiwa.
Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa na kasumba ya kutosimamia mashamba yao pindi wanapoingia shambani hali hii pia inayopelekea Taasisi kupata hasara nakutofikia Malengo ya Uzalishaji.
Alisema wakulima hao wa mkataba wanapaswa kutambua Uzalishaji wa Mbegu ni tofauti na uzalishaji wa chakula hivyo kupitia wataalamu wa ASA wadau hawa watapewa maelezo sahihi pamoja na kuendelea kushauriwa wakati wa zoezi la uzalishaji mbegu mashambani.
Bwn. Leo amewataka wakulima hao kuwa makini katika Uzalishaji wa Mbegu kwani Taasisi hiyo unaweka Malengo ya serikali pamoja na wakulima kutegemea Mbegu hizo ziwafikie sokoni kwa wakati na ubora uliokusudiwa
"Tunataka tuwe makini katika Uzalishaji wa Mbegu hatutaki mzaha mzaha kwani serikali imetupa malengo hivyo ni matumaini yetu mtafanya kazi vizuri pasipo kuwa na changamoto zozote." alisema kaimu Mtendaji Mkuu Bwn Leo Mavika.
Akitoa ufafanuzi wa kisheria mwanasheria wa Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA Valentine Kamugisha amesema lengo la Kikao hicho ni kuwaweka pamoja wakulima wa mkataba na kuwapatia mikataba ili wazalishe mbegu kwa kufuata utaratibu madhubuti wa kisheria.
Amesema Wakala inatarajia kuona matokeo chanya ya Uzalishaji wa Mbegu kuwa makubwa na ya kisasa kutokana na kuingia mikataba ambayo itaweka usawa kati ya Wakala na mkulima.
Aidha amesema baadhi ya wakulima wamekuwa na usumbufu wa udokozi wa Mbegu kwa kupata tamaa ya kuuza Mbegu kama chakula hali inayopelekea Taasisi kupata hasara yakutopata Mbegu kulingana na makadirio yaliyowekwa
Amesema Wakulima wakiwa waaminifu watapewa nafasi ya kulima kila wakati kutokana na historia ya mkulima husika ambayo haina usumbufu.
Amesema Mkulima haruhusiwi kukodisha Shamba alilopewa na Wakala kwa ajili ya Uzalishaji pamoja na kuuza mavuno sehem nyingine tofauti na mkataba unavyomtaka.
"Tunachowaomba kuzingatia mikataba hii haruhusiwi kukodisha ama kuuza Shamba la Wakala na kama ukizalisha Mbegu huruhusiwi kuuza kama Mazao ya chakula nawaomba mzingatie mikataba hii kama mtu akikiuka hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake." alisema mwanasheria wa Taasisi ya Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Valentine Kamugisha.
Mkurugenzi wa Uzalishaji Dkt. Justin Ringo amesema Wakala wa Mbegu ina matumaini makubwa na wakulima hao wa mkataba katika zaoezi hilo la Uzalishaji wa Mbegu.
Amesema matarajio ya Wakala wa Mbegu kuwa wakulima hao wazalishe zaidi ya Tani 7,000 za Mbegu kwa Mazao mbalimbali.
Mkurugenzi wa Uzalishaji amewataka wakulima hao kutokuwa na kilimo cha mitandaoni badala yake watenge muda wa kutembelea Mashamba yao ilikuepuka hasara zinazoweza kujitokeza kwa kutotembelea Shamba.
Aidha Dkt. Ringo amewataka wakulima hao kuzingatia kanuni za Uzalishaji wa Mbegu bora hasa kupanda na kuvuna kwa wakati, utunzaji mazao, usafi wa mbegu pamoja na uhifadhi kabla ya kusafirisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakulima wa mkataba wameipongeza Wakala wa Mbegu ASA Kwa kufanya kazi na wakulima wa mkataba dhidi ya Uzalishaji wa Mbegu bora za kilimo.
Mwambambale Asajile mkulima wa mkataba Shamba la Mbegu Kilangali amesema Kikao hicho cha wakulima na Wakala ni Kikao kizuri kinacholenga kuimarisha ushirikiano wa Uzalishaji wa Mbegu ili kuongeza Uzalishaji Nchini.
Amesema Wakulima hao watafanya kazi kwa kuzingatia mikataba inavyosema ili kufikia Malengo na kuongeza kuwa Wakala wa Mbegu unapaswa kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ainishwa na wakulima hao. Aidha, ameishukuru ASA kwa kuwakutanisha na watoa huduma za kifedha.
Mwisho.