emblem

ARDHI UNIVERSITY

News and Events

Wanakijiji wapongeza mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu Ardhi tawi la Mwanza

 

Wakazi wa kijiji cha Karumo ambako kampasi mpya ya Chuo Kikuu Ardhi inajengwa, wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia (WyEST) kwa kujenga Chuo kitakachokua kinafundisha programu mbalimbali za ujuzi kwa ngazi ya Stashahada na Shahada.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 9 Mei, 2023 na Mwenyekiti wa kijiji Ndg. Tiba Magambo kwenye eneo la Kampasi hiyo wakati wa Ziara ya wanahabari kwenye ujenzi huo unaotekelezwa na Chuo Kikuu Ardhi kupitia Mradi wa HEET unaosimamiwa na WyEST. 

Ndg. Magambo ameshukuru Chuo kwa kutoa fidia kwa wakati ambayo imewezesha wakazi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba bora.“ Wanakijiji waliokuwa na nyumba duni wameboresha makazi yao na waliokuwa hawana wamejenga nyumba za kuishi” amesema ndg. Magambo.

Kwa upande wake mratibu msaidizi wa mradi wa HEET Taifa Dkt. Evaristo Mtitu amesema Programu zitakazotolewa kwenye Kampasi hiyo zinalenga kutoa Elimu ujuzi itakayomsaidia mhusika kuweza kujitegemea na kuleta mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.

Nae Mratibu wa maswala ya ujenzi HEET ARU Dkt. Fredrick Salukele  amesema Kampasi hiyo ina ukubwa wa ekari 378 na kwa kuanzia yatajengwa majengo matano (5) Jengo la madarasa na studio; Jengo la Utawala, Mabweni ya wanafunzi, Zahanati na Jengo la nyumba za makazi ya wakufunzi). Majengo yote hayo yatakua na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,720 na familia 8 za wakufunzi, mabweni kwa wanafunzi 412 na ofisi kwa wafanyakazi 131.